Alhamisi 18 Juni 2026 - 19:54
Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia wa Lebanon Latoa Maelekezo Kuhusu Majlisi za Maombolezo ya Muharram

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Ali Al-Khatib, Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia wa Lebanon, ametoa taarifa maalumu kwa mnasaba wa maombolezo ya mwezi wa Muharram.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Ali Al-Khatib, Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia wa Lebanon, katika taarifa yake kuhusu maombolezo ya mwezi wa Muharram alisema: “Muharram ya mwaka huu inakuja katika mazingira magumu na yenye changamoto kubwa ambayo watu wetu wameyapitia na bado wanaendelea kukabiliana nayo kutokana na uvamizi wa kinyama wa Marekani na Israel pamoja na athari zake, zikiwemo kuhama kwa lazima, kufukuzwa kutoka makazi yao, kukosa makaazi, wingi wa mashahidi na uharibifu mkubwa katika maeneo yetu, miji yetu na vijiji vyetu, uliosababishwa na uvamizi wa kinyama na usio wa kiungwana wa Kizayuni.”

Aliongeza: “Hali hii haitatuzuia kuhuisha tukio hili, bali itakuwa sababu ya kutupa hamasa zaidi na kusisitiza kulifanikisha, kwa sababu tukio hili linaakisi fikra zetu, utambulisho wetu wa kitamaduni, uhusiano wetu wa kidini na wa kiustaarabu, kwa mujibu wa mwenendo wa Ahlul-Bayt (as). Hivyo basi, katika tukio hili tunatoa mkono wa pole kwa watu wetu kwa kumbukumbu ya kuuawa kishahidi Sayyidush-Shuhadaa, mjukuu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Imam Hussein (as), pamoja na Ahlul-Bayt wake na masahaba wake.

Tunathamini msisitizo wenu wa kuhuisha nembo hizi za dini hata katika mazingira haya ya hatari na migogoro, kwa sababu huu ndio mwelekeo ambao mmelelewa juu yake na misingi yake ndiyo iliyowapa nguvu na irada ya kukabiliana na dhulma na uvamizi katika kipindi chote cha historia.

Katika kuendeleza njia hii, nyinyi wanaume na wanawake wa leo, pamoja na watoto wenu wa muqawama, mnarejesha upya taswira za ushujaa, heshima, utukufu, subira, azma na ustahimilivu katika vita vya kulinda heshima, vinavyoendelea katika vilima, mabonde na fukwe za Jabal Amil, kwa kumfuata Sayyidush-Shuhadaa pamoja na dada yake mtukufu Bibi Zainab (sa), shujaa wa Karbala, na kundi la Ahlul-Bayt wake na masahaba wake.”

Aliendelea kusema: “Watu wetu waliobaki katika maeneo yao pamoja na wale waliofukuzwa kwa dhulma kutoka katiks nyumba zao wanaitwa mwaka huu kuandaa na kushiriki katika Majlisi za maombolezo ya Muharram kwa kuzingatia hali zilizopo kwa sasa; kwa upande mmoja kwa ajili ya kulinda usalama wao, na kwa upande mwingine kwa kuheshimu maeneo wanayoishi, huku wakizingatia maelekezo yafuatayo:”

Kwanza: Tathmini ya uwezekano wa kuandaa Majlisi za maombolezo za Muharram na namna ya kuzitekeleza katika maeneo yanayoweza kushambuliwa kwa mabomu itaamuliwa na waandaaji wa Majlisi hizo wenyewe.

Pili: Waandaaji wa Majlisi katika maeneo salama wanatakiwa kuzipanga kwa utaratibu unaostahiki, na kwa kushirikiana na waratibu na vikosi vya kijeshi na vya usalama wachukue hatua za kiusalama zinazohitajika. Aidha, wanapaswa kujiepusha kabisa na kuwasumbua wakazi kwa matumizi ya vipaza sauti.

Tatu: Kuepukana na kuandaa Majlisi nje ya maeneo yaliyotengwa rasmi kwa shughuli hizo, na shughuli hizo zibakie ndani ya maeneo yaliyofunikwa, pia, kuepukana na kusimamisha mabango na bendera nje ya maeneo ya kufanyia Majlisi za maombolezo.

Nne: Kuepukana na kuandaa maandamano ya jadi, hususan maandamano ya pikipiki.

Tano: Inapendekezwa Majlisi zifanyike wakati wa mchana na kabla ya machweo ya jua, na zisiepushwe kufanyika nyakati za usiku.

Sita: Wahadhiri na waombolezaji wa Majlisi wanatakiwa kusisitiza umoja wa kitaifa wa ndani na, kwa kuongozwa na mwenendo wa Amirul-Muuminin Ali bin Abi Talib (as), Imam Hussein (as) na Maimamu Watoharifu (as) kuhusu umoja wa Umma, wajiepushe na maneno ya kimadhehebu na ya uchochezi.

Mwishoni mwa taarifa yake, Sheikh Ali Al-Khatib alisema: “Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia linategemea uelewa wa watoto wetu kuhusu maelekezo haya na kushikamana nayo. Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awajumuishe mashahidi wetu pamoja na mashahidi wa Karbala, awape watu wetu subira na utulivu, awaponye majeruhi wetu, awaachilie huru mateka wetu, na awawezeshe watu wetu kurejea kwa heshima katika vijiji na nyumba zao, hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuitikia maombi.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha